Makonda akabidhi ramani ya ofisi mpya za Bakwata

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekabidhi ramani ya jengo la kisasa la ghorofa tatu litakalokuwa ofisi ya Mufti wa BAKWATA nchini litakalojengwa kupitia wafadhili mbalimbali na litagharimu shilingi bilioni 5.08.
Amekabidhi ramani hiyo Jumatatu hii katika hafla iliyofanyika baada ya sala ya adhuhuri katika viwanja vya BAKWATA Kinondoni jijini Dar es salaam.
“Leo nimefika hapa ikiwa ni mwanzo wa safari mpya ya serikali ya mkoa wa Dar kujenga makao makuu mpya ya kisasa ya ndugu zangu, viongozi wangu wa BAKWATA, najua watu wote wana viongozi kama baba ni kiongozi wa familia, watu wana vyama vyao vya siasa wana viongozi,watu wana makampuni yao wana viongozi lakini viongozi hawa wanatofautiana na viongozi wa dini kwa jambo moja, viongozi wa dini wanatuongoza kutupeleka kwa mola alietuumba sote”, alisema Makonda
Kwa upande wake Mufti mkuu wa Dar es Salaam, Abubakar Zubeir alisema, “kila mwenye uwezo wa kuweza kusaidia jambo hili basi anyooshe mkono kusaidia, hakuna jambo ambalo linafaa kusaidia kama mambo ya heri na ya Kimungu, ukisaidia jambo la kimungu umesaidia Mungu apatikane pale, watu kumtaja Mungu pale, umesaidia watu kumjua Mungu, utakuwa umesaidia watu kujifunza maadili mema na pia utasaidia mambo ya kulinda amani na kutunza nchi,” alisema Mufti huyo.
Naye Sheikh mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum alisema, “leo tunashuhudia Makonda anakuja kufanya kitu ndani ya makao makuu ya BAKWATA hizi harakati zinatokana na wazazi wako wako waliokulea inaonyesha baraka kubwa,vitu hivi vinakuwa vya baraka.”
Makonda alimaliza kwa kusema viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuhamasisha amani na kulinda amani. Mwishoni masheikh walikuwa na dua maalum ya kumuombea mkuu huyo wa mkoa.
BY: EMMY MWAIPOPO

0 maoni:

Chapisha Maoni