Watoto wamiminika katika kambi ya tiba ya vichwa vikubwa na mgongo wazi Songea

Zaidi ya watoto 50 Jumapili hii wamehudhuria kambi tiba ya GSM Foundation inayoendeshwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Mifupa na upasuaji ya MOI, yenye lengo la kupunguza vifo na mtindio wa ubongo kwa watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi, ambayo leo imeingia katika mkoa wa pili katika msimu wake wa pili pia, wenye lengo la kuwafanyia upasuaji watoto 100.
Wagonjwa wakisajiliwa katika chumba maalum cha kuwapokea katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma

Kaimu Mkuu wa kambi hiyo iliyoanzia mkoani Mtwara Jumanne ya tarehe 2 mwezi huu, DK Shaaban Hamis, amesema, muitikio walioupata katika mkoa huu ni muitikio mkubwa zaidi ukilinganisha na mkoa wa Mtwara, ambako ndio kunakosadikika kuwa na wagonjwa wengi zaidi, kutokana na rekodi waliyonayo, baada ya tafiti mbali mbali.
“Inawezekana hapa tukafanyia upasuaji wagonjwa hata 50 kwa siku hizi tatu tutakazokuwepo, na labda tukavuka lengo katika mikoa iliyobaki ya Iringa na Mbeya ambayo ndio ya mwisho katika msimu huu wa pili”, alisema Dk Shaaban.
Kwa upande wake Afisa uhusiano wa Taasisi ya GSM ambayo kwa mwaka huu imewekeza zaidi kusaidia sekta ya Afya na Elimu, Khalphan Kiwamba amesema wanafarijika kuona wagonjwa wanakwenda kutibiwa kama walivyodhamiria, maana ndio lengo haswa, kusaidia kupunguza vifo vya watoto ambao wanasadikika kuzaliwa 4000, kwa mwaka lakini kati yao, ni asilimia 25 tu hurudi hospitalini kwa matibabu huku asilimia 75 wakishindwa kutokana na sababu za kiuchumi.

0 maoni:

Chapisha Maoni